Nchi zaidi ya thelathini kushiriki maonyesho ya utalii Tanzania
2024-10-14 13:50:12| cri

Takriban nchi 33 zimethibitisha kushiriki maonyesho ya kimataifa ya utalii ya Swahili International Tourism Expo (Site) yanayotarajia kufanyika nchini Tanzania wiki hii.

Maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Tanzania kuwa na uwezo wa kufikia masoko katika nchi ambazo bado hazijaleta watalii wengi licha ya kuwa na watu wengi.

Maonyesho hayo yanabebwa na kauli mbiu isemayo, “Tembelea Tanzania kwa uwekezaji endelevu na utalii usio mithilika.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema uwepo wa maonyesho hayo unalenga kuimarisha mtandao wa wafanyabiashara waliopo katika sekta ya utalii wa ndani na nje ya nchi.

Amesema tayari wamepokea uthibitisho wa ushiriki wa wadau 145 kutoka nchi 33 na kati yake zipo nchi ambazo ni masoko ya kimkakati.

Baadhi ya nchi zilizothibitisha ushiriki ni China, Denmark, Finland, Japan, Afrika Kusini, Kenya, Ethiopia, India, Oman, Uholanzi, Nigeria, Brazil, Ujerumani, Uganda na Lesotho.

Miongoni mwa mambo yatakayofanyika ndani ya siku hizo tatu katika ukumbi wa Mlimani City ni kuonyesha mazao ya biashara yaliyopo katika sekta ya utalii ili wanunuzi wakutane na wazalishaji kuendeleza mnyororo mzima.