Tiba za asili na umuhimu wake katika mfumo wa huduma za afya
2024-10-18 08:34:36| CRI

Kwa karne nyingi, maarifa ya kimapokeo na asilia ya mababu zetu yamekuwa nyenzo muhimu kwa afya katika kaya na jamii, na yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya huduma ya afya katika maeneo mengi. Mataifa 170 kati ya 194 Wanachama wa WHO yameripoti kuhusu matumizi ya dawa za mitishamba, acupuncture, yoga, tiba asilia na aina nyinginezo za dawa za kienyeji. Nchi nyingi zinatambua tiba asilia kama chanzo muhimu cha huduma ya afya na zimechukua hatua za kuunganisha matibabu yake, bidhaa zake na matabibu wake katika mifumo yao ya kitaifa. Hivi sasa dawa za jadi zimekuwa jambo la kimataifa, ambapo mahitaji yake yanaongezeka kila siku.

Kwa mamilioni ya watu, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya mbali na vijijini, tiba za asili zinaendelea kuwa chaguo la kwanza kwa afya na ustawi, na kutoa huduma ambayo inakubalika, inapatikana na ya bei nafuu. Kazi ya WHO kuhusu tiba asili ni kushughulikia na kujibu maombi ya nchi husika ambayo yana ushahidi na data zinazofafanua sera na matibabu na viwango, na kanuni za kimataifa ili kuhakikisha usalama, ubora na ufikiaji sawa. Azimio la 2018 la Astana kuhusu huduma ya afya ya msingi linatambua haja ya kujumuisha maarifa ya tiba za asili na teknolojia katika utoaji wa huduma ya afya ya msingi ili kuweza kufikia huduma ya afya kwa wote. Katika kipindi cha ukumbi wa Wanawake leo tutajadili tiba za asili na umuhimu wake katika mfumo huduma za afya.