Walinda amani wa Umoja wa Mataifa waendelea kubaki katika maeneo yao nchini Lebanon
2024-10-15 08:55:53| CRI

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na operesheni za ulinzi wa amani Jean-Pierre Lacroix amesema, askari wa kulinda amani wa Umoja huo wataendelea kubaki katika sehemu zao nchini Lebanon.

Akizungumza baada ya kutoa taarifa fupi kuhusu hali ya Lebanon kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Lecroix amesema uamuzi umefikiwa kwamba Tume ya Mpito ya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) itaendelea kubaki katika maeneo yake licha ya wito uliotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Israel kuwataka kuondoka katika nafasi hizo zilizo katika Mstari wa Blue kati ya Lebanon na Israel.

Wakati huohuo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu mapigano yanayoendelea katika eneo la Mstari wa Blue.

Nchi wajumbe wa Baraza hilo wamezitaka pande zote husika kuheshimu usalama wa askari wa UNIFIL na maeneo ya Umoja wa Mataifa, na kurejea tena uungaji mkono wao wa tume hiyo, huku wakisisitiza nafasi yake muhimu katika kuleta utulivu wa kikanda.