Wakenya sasa wataweza kutuma pesa kwenda Ethiopia kwa kutumia M-Pesa kupitia Safaricom Kenya na tawi lake la Ethiopia.
Upanuzi wa huduma ya M-Pesa Global unalenga kuongeza matumizi ya pesa za kielektroniki nchini Ethiopia, hivyo kusaidia uchumi wa wa taifa hilo na mataifa mengine ya bara Afrika.
Esther Waititu, Afisa Mkuu wa Huduma za Fedha wa Safaricom Kenya, amesema kwamba ushirikiano huu unadhihirisha dhamira yao ya kutoa suluhu za kifedha pamoja na huduma zinazokidhi mahitaji yanayobadilika ya wateja wao kibiashara.
Huduma hii itapatikana kwenye pochi ya M-Pesa na kwa wateja wote wa Safaricom nchini Ethiopia kupitia M-Pesa International Remittance.
Kwa kuongeza, wateja wa M-Pesa wanaweza kutuma na kupokea pesa katika zaidi ya nchi 190. Elsa Muzzolini, Afisa Mkuu wa Huduma za Fedha wa Safaricom Ethiopia, aliongeza kwamba ushirikiano huu utawezesha wateja wa M-Pesa Ethiopia kupokea matangazo salama na ya gharama nafuu kutoka Kenya, hivyo kukuza matumizi ya malipo ya kidijitali katika eneo hilo.
Wataalam wa masuala ya fedha wanasema hatua hiyo ni muhimu kwani itasaidia pakubwa katika kuboresha uchumi na biashara baina ya Kenya na Ethiopia.