Mkutano muhimu wa siku mbili umeanza jana katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kutafuta njia za kudumisha mageuzi ya kiuchumi nchini humo.
Mkutano wa 7 wa Sera za Uchumi za Kitaifa uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, unalenga kujadili na kuboresha maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo na fursa za uwekezaji ndani ya sekta mbalimbali.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Barre amesisitiza haja ya kuwekeza katika ujuzi na ubora wa watu wa Somalia ili kujenga uchumi nymbufu, na kuongeza kuwa, Somalia inakabiliwa na changamoto zinazozuia ukuaji wa uchumi, ingawa ina fursa nyingi ambazo bado hazijatumika ipasavyo.
Mkutano huo ulioandaliwa na Kamati ya Uchumi ya Kitaifa (NEC), utawawezesha washiriki kutafiti vipaumbele baada ya kusamehewa madeni, ikiwemo usimamizi wa fedha za umma, kuzuia ongezeko la madeni, na kutumia vizuri msamaha wa madeni kuongeza uwajibikaji wa bajeti ya serikali na ukuaji wa uchumi.