Bodi ya Utalii ya Kenya (KTB) imeanzisha kampeni mpya itakayoweza kuongeza idadi ya watalii wanaofika nchini Kenya, ikitumia balozi na vituo vya Kenya katika nchi za kigeni.
Kampeni hii, iitwayo ‘Ziara Kenya: One Diaspora, One Tourist,’ inawalenga Wakenya zaidi ya milioni 3 walio nje ya nchi kuhamasisha utalii kupitia mitandao yao na kuboresha biashara ya utalii nchini Kenya.
Mkurugenzi Mtendaji wa KTB, June Chepkemei, alisema kuwa Kenya ina balozi 66 ambazo zinawakilisha nchi na kwamba miundombinu hii inatoa fursa bora ya kuweka Kenya kama kivutio kikuu kwa wasafiri wa kimataifa pamoja na kivutio cha wawekezaji wa kibiashara.
Kampeni hii inalenga kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.9 hadi milioni 5 ifikapo mwaka 2027, hivyo kuimarisha nafasi ya Kenya katika midani ya utalii.
Chepkemei alisisitiza kuwa KTB itawapa Wakenya wanaoishi nje ya nchi motisha ili kuhamasisha utalii katika mitandao yao ya kijamii, ikifanya kazi na sekta ya usafiri kuleta mabadiliko haya.