Naibu balozi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Geng Shuang tarehe 15 alipohutubia mkutano wa Baraza la Usalama la UM kuhusu suala la Yemen alisisitiza kuwa, mazungumzo ni njia sahihi ya kipekee ya kutatua suala la Yemen.
Balozi Geng Shuang amesema katika wiki kadhaa zilizopita, mapambano katika Ukanda wa Gaza yanaendelea, hali kati ya Lebanon na Israel imezidi kuwa mbaya. Kundi la Houthi la Yemen limefanya mashambulizi dhidi ya Israel, na Israel imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya bandari ya Hodeidah na Ras-Isa. China imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya sasa na mwelekeo wa huko, na kuona kuwa jambo muhimu kwa sasa ni kutuliza hali ya wasiwasi, na kuzuia kuongezeka kwa mapambano. China inatoa wito kwa pande zote husika zijizuie na kuepuka kitendo chochote kinachoweza kuchochea hali kuwa ya wasiwasi zaidi.
Ameongeza kuwa China inatoa wito kwa pande zote husika kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo, na kuunga mkono kazi ya mjumbe maalumu wa UM anayeshughulikia suala la Yemen.