Biashara ya nje ya China yakua zaidi ya makadirio
2024-10-16 11:03:37| cri

Takwimu zimeonesha kuwa katika robo tatu za mwanzo za mwaka huu, thamani ya bidhaa zilizoagizwa na kuuzwa nje ya China ilikuwa Yuan trilioni 32.33, ikiongezeka kwa 5.3% ikilinganishwa na mwaka jana. Kati yake, mauzo ya nje yaliongezeka kwa 6.2% na uagizaji kutoka nje uliongezeka kwa 4.1%. Maoni ya kimataifa yanaonesha kuwa katika mazingira ambayo uchumi wa dunia bado unafufuka na vitendo vya kujilinda kibiashara kimataifa vinaongezeka, si jambo rahisi kwa biashara ya nje ya China kufanikiwa kutimiza ukuaji uliozidi makadirio. 

Kinachostahili kuzingatiwa ni kuwa katika "ripoti hii ya matokeo", kuna "mara ya kwanza" mbili: kwanza, katika robo tatu za mwanzo za mwaka huu, thamani ya uagizaji na uuzaji nje wa bidhaa ilizidi Yuan trilioni 32 kwa mara ya kwanza katika historia, ikiongezeka kutoka Yuan trilioni 30.8 za mwaka jana kwa wakati huo; pili, thamani ya uagizaji na uuzaji nje wa bidhaa ilizidi Yuan trilioni 10 katika kila robo ya mwaka, ikionyesha ongezeko robo baada ya nyingine, hali ambayo pia ni ya "mara ya kwanza" katika historia kwa kipindi hicho. Ikilinganishwa na hali hiyo, thamani ya uagizaji na uuzaji nje wa bidhaa katika robo tatu za mwanzo za mwaka jana ilikuwa Yuan trilioni 9.72, trilioni 10.29, na trilioni 10.79 mtawalia.

Mafanikio hayo yalitokana na nini? Kwa upande wa ndani, bidhaa za China zina ushindani mkubwa kutokana na minyororo kamili ya ugavi wa tasnia ya utengenezaji, athari za uchumi wa kiwango kikubwa, na maendeleo ya haraka ya teknolojia, ambavyo vinatoa msingi na uhakikisho wa upanuzi wa soko la kimataifa. Aidha, hali ya kiuchumi ya China ni nzuri, soko lake ni kubwa na lina uthabiti na uwezo mkubwa. 

Kwa upande wa nje, mahitaji ya nje yameongezeka hivi karibuni, na hii imeweka mazingira mazuri kwa mauzo ya nje ya China. Hivi karibuni, Shirika la Biashara la Kimataifa limeongeza utabiri wa ongezeko la biashara ya bidhaa kwa mwaka mzima, na mashirika ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo yanaamini kuwa uchumi wa dunia umeanza kuimarika. Katika hali hii, katika robo tatu za mwanzo za mwaka huu, mauzo ya China kwa masoko ya jadi kama vile Ulaya, Marekani na Japan yaliongezeka kwa 4.2%, na mauzo kwa masoko yanayojitokeza kama jumuiya ya ASEAN na Amerika ya Kusini yaliongezeka kwa 12.3% na 13.7% mtawalia.