Msemaji wa Rais wa Nigeria Bayo Onanuga amesema, watu zaidi ya 100 wamefariki kufuatia mlipuko wa lori la mafuta katika mji wa Majiya ulioko wilaya ya Taura mkoani Jigawa, kaskazini mwa nchi hiyo mapema wiki hii.
Taarifa iliyotolewa na msemaji hiyo jumatano jioni kwa niaba ya rais wa Nigeria Bola Tinubu, imesema rais Tinubu ametoa maelekezo kwa maofisa wa ngazi ya juu kutoa rambirambi kwa familia za marehemu, kufanya tathmini ya hali ilivyo katika eneo la tukio, na kuwatembelea watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo ambao wamelazwa hospitali.
Pia ametoa maelekezo kuhusu msaada wa dharura unaojumuisha upatikanaji wa vifaa vya matibabu, chakula, na hifadhi vipelekwe kwa majeruhi walioko hospitali na watu wengine walioathirika na mlipuko huo.