Mkurugenzi wa WHO Afrika aipongeza Rwanda kwa hatua zake za kukabiliana na mlipuko wa Marburg
2024-10-17 10:46:51| cri

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, ameitembelea Rwanda na kujionea kazi ya kupambana na mlipuko wa homa ya Marburg mjini Kigali, na kuwashukuru wafanyakazi wa afya wa Rwanda na watu walionusurika kutokana na kazi yao na ujasiri.

Dkt. Moeti aliwasili nchini Rwanda Jumanne kushuhudia hatua zinazoendelea za kupambana na ugonjwa wa Marburg na ushirikiano kati ya WHO na serikali ya Rwanda. Dkt. Moeti amesema kupitia mtandao wa X kuwa amefurahishwa na hatua ya Rwanda ya kuchukua hatua za haraka kutambua wagonjwa, na kutoa huduma bora za kimatibabu ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kwenye mkutano na Waziri wa Afya Dkt. Sabin Nsanzimana, Dkt. Moeti ameipongeza Serikali ya Rwanda kwa hatua zake, na kusisitiza ahadi ya WHO kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ya nchi hiyo ili kuzuia mlipuko huo.