Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeanzisha mikakati mbalimbali ya kuimarisha miundombinu ya nishati katika ukanda huo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza ushirikiano na kuhakikisha umeme wa uhakika na wa bei nafuu.
Mkutano wa 57 wa Kamati ya kuchangia Umeme ya Kusini mwa Afrika (SAPP) ya SADC, umefanyika jijini Dar es Salaam ukijadili namna nchi wanachama zinavyoweza kushirikiana katika kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme kwa ufanisi kwa lengo la kupunguza gharama za nishati na kuboresha biashara ya umeme katika kanda nzima.
Mbali na mwenyeji Tanzania, nchi nyingine zilizoshiriki kwenye mkutano huo ni Malawi, Zambia, Angola na Zimbabwe, zikieleza mikakati ya kuzalisha umeme wa kutosha, kuunganisha gridi za umeme za kikanda na kutumia vyanzo mbadala kama vile nishati ya jua, upepo na nishati ya mvuke.