Waziri wa Afya wa Rwanda Bw. Sabin Nsanzimana amesema kwa muda wa siku tano zilizopita hakuna maambukizi mapya ya ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) nchini humo, hali inayoashiria kuwa hatua kubwa zimepigwa katika mapambano dhidi ya virusi hivyo nchini Rwanda.
Bw. Nsanzimana ametoa taarifa hiyo wakati wa mkutano na wanahabari mjini Kigali, wakati nchi hiyo ikiendelea na juhudi za kudhibiti kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.
Amesema kati ya watu 62 walioambukizwa ugonjwa huo, 15 wamefariki dunia na wengi wamepona, kwa sasa ni wagonjwa watatu tu ambao bado wanaendelea na matibabu.
Dk. Nsazimana amesema Rwanda itaendelea kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuimarisha ufuatiliaji na mwitikio, ili kuhakikisha inajiandaa vizuri dhidi ya uwezekano wa kutoka kwa maambukizi yoyote.