Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Lebanon yafikia 2,464 na 11,530 wamejeruhiwa
2024-10-21 13:58:58| cri

Wizara ya afya ya Lebanon imeripoti kuwa idadi ya watu waliofariki kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Lebanon tangu kuanza kwa mgogoro kati ya Israel na kundi la Hezbollah imefikia 2,464, na idadi ya majeruhi imeongezeka hadi 11,530.

Wizara hiyo imesema katika siku ya Jumamosi pekee watu 16 waliuawa na wengine 59 walijeruhiwa katika mashambulizi ya Israel.

Kuanzia tarehe 23 Septemba, jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya Lebanon na mgogoro kati yake na kundi la Hezbollah umeongezeka. Tangu Oktoba 8, mwaka jana kundi la Hezbollah na jeshi la Israel wamekuwa wakipambana kwenye mpaka wa Lebanon na Israel huku kukiwa na hofu ya kutokea mgogoro mkubwa wakati vita kati ya kundi la Hamas na Israel ikiendelea katika Ukanda wa Gaza.