Mamlaka ya mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania imesema mtu mmoja amefariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na wengine 25 wamelazwa katika vituo vya afya baada ya kuambukizwa ugonjwa huo.
Ofisa wa afya mkoa wa Lindi Bw. Kheri Kagya amesema, mlipuko wa kipindupindu uliripotiwa Oktoba 13 katika kijiji cha Zinga Kibaoni wilayani Kilwa.
Bw. Kagya amesema hii ni mara ya pili kwa mlipuko huo kuripotiwa mkoani Lindi, baada ya kuripotiwa kwa mara ya kwanza Septemba 17.
Amesema mamlaka katika mkoa huo zilifanikiwa kudhibiti mlipuko wa kwanza wa ugonjwa huo kabla ya kusababisha madhara makubwa. Wafanyakazi wa afya wanafanya kazi usiku kucha ili kudhibiti mlipuko wa pili.