Wataalamu wa afya wa Afrika wakutana Uganda kujadili mwitiko wa homa ya Mpox
2024-10-22 09:28:52| CRI

Wataalamu kutoka nchi za Afrika zilizoripoti milipuko ya homa ya mpox, pamoja na mashirika ya afya ya kikanda, walikutana Jumatatu mjini Kampala, Uganda kutathmini mwitikio wa kuvuka mpaka wa kudhibiti homa hiyo.

Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Uganda imesema kupitia mtandao wa X kuwa wataalamu kutoka nchi kumi za Afrika, Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Afrika (Africa CDC), na Ofisi ya WHO kanda ya Afrika, wamekutana kujadili ushirikiano wa kimataifa wa kuzuia kuenea kwa homa hiyo.

Kwa mujibu wa Africa CDC, idadi ya vifo kutokana na milipuko inayoendelea ya homa ya Mpox imepita 1,100, huku kukiwa na watu 42,438 wanaoshukiwa kuambukizwa katika nchi 18 za Afrika, kati yao watu 8,113 wamethibitishwa kuambukizwa homa hiyo, tangu mwanzo wa mwaka huu.