Umoja wa Afrika umelaani vurugu na mauaji yaliyotokea hivi karibuni nchini Msumbiji baada ya uchaguzi mkuu na kuzitaka pande zote nchini humo kutulia.
Kwenye taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa Moussa Faki Mahamat, umoja huo umeeleza wasiwasi juu ya matukio ya vurugu hiyo na kutoa rambirambi kwa familia za wahanga wawili waliouawa hivi karibuni. Habari zinasema watu hao wawili wenye uhusiano na mgombea urais Venancio Mondlane waliuawa kwa kupigwa risasi mjini Maputo wakati wa mvutano baada ya uchaguzi nchini humo.
Bw. Mahmat ametaka mamlaka ya usalama ya Msumbiji kufanya uchunguzi na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria, na pia ametoa wito kwa pande zote za kisiasa nchini humo kutulia na kujizuia wakati wakisubiri matokeo rasmi yatakayotangazwa na Baraza la Kikatiba na kuruhusu mchakato unaostahili kwa maslahi ya jumla ya utulivu nchini humo.