Wanafunzi zaidi ya 40 walazwa hospitali kutokana na kuhisiwa kula chakula chenye sumu Afrika Kusini
2024-10-23 23:57:34| cri

Idara ya elimu ya mkoa wa KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini Jumanne ilithibitisha kuwa wanafunzi 43 wa shule ya msingi mkoani humo Jumatatu walipelekwa hospitalini kutokana na kuhisiwa kula chakula chenye sumu.

Idara hiyo ilisema wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ngaqa huko Mtubatuba waliumwa baada ya kula vitafunwa vilivyouzwa mtaani nje ya shule.

Katika siku za karibuni Afrika Kusini imeshuhudia ongezeko kubwa la matukio ya sumu kwenye chakula miongoni mwa watoto. Tarehe 6 Oktoba watoto sita walikufa kwa kuhisiwa kula chakula chenye sumu huko Johannesburg. Mapema mwezi huu, wanafunzi zaidi ya 130 wa mkoa wa Gauteng, Limpopo, na KwaZulu-Natal walilazwa hospitali kutokana na sababu zinazofanana.