Tanzania na kampuni ya China zasaini makubaliano ya ujenzi wa daraja la mita 390
2024-10-24 09:25:11| CRI

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC) zimesaini makubaliano ya ujenzi wa daraja la mita 390 kwenye eneo la Jangwani mjini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya ujenzi, imesema wakala wa barabara wa Tanzania TANROADs imetia saini makubaliano hayo na kampuni ya China kwa niaba ya serikali, huku hafla ya utiaji saini ikishuhudiwa na waziri wa ujenzi Bw. Innocent Bashungwa.

Ujenzi wa daraja hilo lenye thamani ya dola za kimarekani milioni 36 utakwenda sambamba na ujenzi wa kuta za kulinda kingo za Mto Msimbazi, kutokana na eneo la daraja hilo kuweza kukumbwa na mafuriko nyakati za mvua. Mradi huo utasimamiwa na ofisi ya rais inayoshughulikia tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Daraja la Jangwani likikamilika litatoa unafuu kwa zaidi ya madereva 500,000 wanaotumia daraja hilo kila siku.