Rais Xi akutana na mwenzake wa Misri El-Sisi
2024-10-24 10:13:02| cri

Rais Xi Jinping wa China Jumatano usiku alikutana na mwenzake wa Misri Abdel Fattah El-Sisi kando ya mkutano wa 16 wa kilele wa BRICS uliofanyika mjini Kazan, Russia.

Rais Xi ameipongeza na kuikaribisha Misri kushiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa viongozi wa nchi za BRICS kama mwanachama rasmi. Rais Xi amebainisha kuwa huu ni mwaka wa kumi tangu China na Misri zianzishe uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote. China inaiunga mkono kithabiti Misri kulinda mamlaka, usalama na maslahi yake ya maendeleo, na inapenda kuwa rafiki wa dhati na mshirika wa karibu wa maendeleo wa Misri.

Kwa upande wake Rais El-Sisi amesema katika muongo uliopita tangu Misri na China zilipoanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote, nchi hizo mbili zimepata matunda mengi ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Rais El-Sisi ameishukuru China kwa kuiunga mkono Misri kujiunga na BRICS, na Misri inapenda kushirikiana kwa karibu na China katika kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea na nchi za Dunia ya Kusini, na kusukuma mbele ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa dunia ulio wa haki zaidi.