Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) jana Alhamisi liliahidi kuunga mkono programu ya kitaifa ya Kenya ya kutoa chanjo ya polio ili kutokomeza mlipuko wa ugonjwa huo nchini humo.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Kenya Shaheen Nilofer amesema kupitia taarifa kuwa programu hiyo inajitahidi kufikia lengo la kutoa chanjo ya polio kwa asilimia 88 ya watoto nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mlipuko wa sasa wa polio nchini Kenya unachochewa na mchanganyiko wa sababu, ikiwemo janga la Uviko-19 ambalo lilisitisha utoaji wa huduma za kawaida za chanjo na mfumo wa afya.
Taarifa hiyo imekuja baada ya Wizara ya Afya ya Kenya kusema Oktoba 19 kuwa watoto wasiopungua milioni 3.71 wamepewa chanjo ya polio katika juhudi za serikali ya nchi hiyo kutokomeza ugonjwa huo.