Rais William Ruto wa Kenya amewataka wawekezaji binafsi kuchunguza kikamilifu uwepo wa nishati ya joto ardhi nchini Kenya, akibainisha kuwa ni asilimia 10 tu ya eneo la Kenya ndio limefanyiwa uchunguzi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 35 (MW) katika eneo la Menengai, Nakuru, Ruto amesema hadi sasa ni MW 950 tu zimepatikana, ambazo ni sehemu ndogo ya uwezo wa jumla wa karibu MW 10,000, na fursa kubwa bado haijatumiwa.
Kampuni ya Kaishan Group ya China imewekeza dola za kimarekani milioni 93 kwenye mradi huo, ambao unatarajiwa kujengwa kwa muda wa miezi 17, na kuhimiza hatua ya Kenya kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi na kuongeza uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.