Wanawake wanavyobana matumizi ya familia
2024-10-26 09:00:02| CRI

    Inafahamika kwamba wanawake ni kundi ambalo wanapenda sana kufanya manunuzi ya vitu hata vile ambavyo havina umuhimu kwa wakati husika. Mwanamke anaweza kuona kitu akakitamani na kukinunua, lakini anapofika nyumbani, kitu hicho ambacho kilimvutia awali, kinakosa ushawishi, na kubaki kuwa tu pambo. Kwa namna hiyo, anaweza kujikuta akiwa na vitu vingi ambavyo hata havitumii, na matokeo ni kwamba anakuwa amepoteza fedha bure katika manunuzi. Lakini pia, kuna baadhi ya wanawake ambao ni maarufu katika kubana matumizi, yaani wanapitiliza kile kiwango ha kubana matumizi na kuwa wachoyo ama wabahili. Hawa ni wale ambao hata kama ni kitu cha lazima kununua, watajitahidi kadri wanavyoweza kutofanya hivyo mpaka pale itakapofika kuwa hakuna njia nyingine bali kununua.

    Suala hili la kubana matumizi si kwa wanawake tu, bali hata kwa wanaume na vijana wa kike na wa kiume. Ni muhimu kubana matumizi na kujiwekea akiba, lakini si kufanya hivyo kiasi cha kuwa mchoyo ama bahili kama tulivyosema awali. Basi leo katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake, tutazungumzia suala hili la kubana matumizi na kujiwekea akiba, na umuhimu wake kwa mwanamke.