Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri ametangaza kuwa nchi hiyo imetoa pendekezo la kusimamisha mapigano katika Ukanda wa Gaza ili kubadilishana mateka wanne wa Israel na wafungwa kadhaa wa Palestina nchini Israel.
Kwenye mkutano na wanahabari uliohudhuriwa na rais Abdelmadjid wa Algeria ambaye yuko ziarani huko Cairo, rais al-Sisi amesema, katika siku kadhaa zilizopita, Misri imefanya juhudi kubwa kwa kutoa pendekezo linalolenga kuweka hali sawa na kusimamisha mapigano kwa siku mbili ili kubadilishana mateka hao.
Ameongeza kuwa mazungumzo yataanza ndani ya siku 10 ili kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano na kuhakikisha usalama katika usafirishaji wa msaada huko Gaza.
Rais huyo pia amekataza kuwalazimisha wapalestina kuhamia nje ya Ukanda wa Gaza, akionya kuwa Wapalestina wa ukanda wa Gaza wanaendelea kuzingirwa jambo linaloweza kusababisha njaa.