Rais wa Msumbiji atoa wito wa kuungwa mkono kimataifa kufuatia nchi yake kuwa na changamoto baada ya uchaguzi
2024-10-29 10:05:31| CRI

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi Jumatatu alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono nchi hiyo kwa ajili ya kuleta utulivu na amani kufuatia uchaguzi wa hivi karibuni.

Nyusi alitoa wito huo wakati alipokutana na mabalozi wa kigeni huko Maputo, akisisitiza jukumu muhimu la utulivu wa kisiasa katika maendeleo ya Msumbiji na umuhimu wa kulinda amani baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2024.

Nyusi alilaani vikali ghasia za hivi karibuni wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi nchini humo, akisema zimesababisha uharibifu na makabiliano ya moja kwa moja na vyombo vya usalama. Pia alikumbusha muktadha wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, akisema malalamiko yanashughulikiwa na Baraza la Katiba, chombo chenye jukumu la kuthibitisha matokeo ya uchaguzi huo.

Amesisitiza kuwa juhudi za kudumisha utulivu wa ndani zinapaswa kukamilishwa na uungwaji mkono wa kimataifa hasa kutokana na changamoto tata za kiuchumi na kijamii za nchi hiyo.