Bunge la Israel lapitisha sheria ya kupiga marufuku operesheni ya UNRWA nchini Israel
2024-10-29 10:02:34| CRI

Bunge la Israel Jumatatu lilipitisha sheria inayolipiga marufuku Shirika la Msaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina walioko Mashariki ya Kati (UNRWA) kufanya operesheni zake nchini Israel.

Televisheni ya Taifa ya Israel, Kan TV News imeripoti kuwa sheria hiyo mpya iliyopata kura 92 kati ya 120 za wabunge wote, ilipitishwa licha ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kuipinga. Sheria hiyo imesema UNRWA haitaendesha shirika lolote, kutoa huduma, au kufanya shughuli yoyote iwe moja kwa moja au siyo moja kwa moja nchini Israel.

Wakati huohuo, Palestina Jumatatu ililaani kitendo hicho cha bunge la Israel. Shirika la habari la Palestina WAFA liliripoti kuwa msemaji wa rais wa Palestina Nabil Abu Rudeineh alisema kwenye taarifa kuwa, Palestina inakataa na kulaani uamuzi huo, ikisisitiza kuwa inakiuka sheria ya kimataifa na kukosoa maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayolinda uhalali wa kimataifa.