Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametoa mwito wa kufanyika juhudi za kukomesha uadui na kuwalinda raia wa kawaida nchini Sudan inayoathiriwa na vita, akisema kuwa hivi sasa hali hairuhusu kupeleka kikosi cha Umoja huo kwa mafanikio.
Bw. Guterres amesema hayo wakati akijulisha hali ya Sudan kwenye Baraza la Usalama la Umoja huo, akiongeza kuwa miezi 18 imepita tangu mapigano makali yaibuke kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF. Mateso yanaongezeka siku hadi siku, na hivi sasa watu milioni 25 wanahitaji misaada.
Katika hotuba yake, Bw. Guterres amesisitiza vipaumbele vitatu katika kuwalinda raia wa kawaida nchini Sudan. Kwanza, pande mbili zinatakiwa kukubaliana haraka kusimamisha mapigano; pili, watu wa kawaida wanatakiwa kupata ulinzi; na tatu, msaada wa kibinadamu unatakiwa kusafirishwa katika sehemu hiyo.