Kenya Jumanne iliandaa kongamano la 21 la mfululizo wa mihadhara ya China, ambapo washiriki walisisitiza manufaa ya pande zote za ushirikiano kati ya China na Afrika katika kuendeleza maendeleo endelevu kupitia Pendekezo la Ukanda Mmoja Njia Moja.
Naibu mwenyekiti wa zamani wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Erastus Mwencha, alisema Afrika inaweza kupata ufahamu muhimu kutoka kwenye njia ya usasa ya China, kwa kuwa pande zote mbili zinakabiliwa na changamoto zinazofanana za maendeleo na zinaweza kufaidika na masuluhisho ya pamoja.
Ikiwa chini ya kaulimbiu ya "Usasa wa China na Ushirikiano wa hali ya juu wa China na Afrika chini ya Mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja", shughuli hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Sera ya Afrika yenye makao yake makuu mjini Nairobi ikishirikiana na Taasisi ya China na Afrika na Ubalozi wa China nchini Kenya.
Balozi wa Somalia nchini Kenya Jabril Ibrahim Abdulle alizungumzia enzi mpya ya kujiimarisha na mshikamano kote barani Afrika. Naye Zhou Yunfan wa Taasisi ya China na Afrika katika Chuo cha Sayansi ya Jamii cha China amesema usasa ni haki ya nchi zote, pia ni kazi ya pamoja ya China na Afrika baada ya uhuru katika kutafuta maendeleo ya taifa na ustawi wa watu wao.