Serikali ya Tanzania imewekeza Sh bilioni 60 kuboresha bandari tatu kuu za Ziwa Victoria.
Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Erasto Lugenge amewaambia wanahabari waliotembelea bandari za Bukoba na Kemondo, kuwa uwekezaji huo mkubwa katika bandari za Kemondo, Bukoba na Mwanza Kaskazini unatarajiwa kuboresha ufanisi na uwezo wa huduma za usafiri katika eneo hilo.
Maboresho yanayoendelea yanakusudia kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 hadi mita 5 katika Bandari za Kemondo na Bukoba, pia, kuongeza urefu wa gati kutoka mita 75 hadi 92, kuboresha eneo la sakafu kwa kuimarisha muundo wa zege, na kufunga uzio utakaoimarisha usalama.
Maboresho mengine yanajumuisha ujenzi wa maeneo ya kusubiri abiria, vituo vya ukaguzi wa mizigo, mfumo wa umeme wa kisasa, na kinga ya upepo.