Sudan Kusini na IOM wazindua mpango wa kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhu kwa watu waliokimbia makazi yao
2024-10-31 09:54:38| CRI

Sudan Kusini ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Jumatano walizindua mpango wa kutafuta suluhu kwa watu waliokimbia makazi yao unaolenga kusaidia wadau wa masuala ya kibinadamu na maendeleo kuondoka kwenye juhudi za kukabiliana na dharura pekee na badala yake kutekeleza programu ya mpito na ya uokoaji.

Akizungumza wakati wa sherehe huko mjini Juba, mkuu wa Shirika la IOM nchini Sudan Kusini Vijaya Souri alisema mpango huo utawezesha juhudi za pamoja na washirika wao kutoa suluhu kwa watu waliokimbia makazi yao na pia kuweka mipango inayotoa suluhisho ya muda mrefu kwa jamii kuhimili athari za siku zijazo.

Alibainisha kuwa ni muhimu kwao kuwa na uwezo wa kufanya kazi na washirika, kuweza kuondoka kwenye mwitikio wa kibinadamu na kuangalia zaidi suluhu za mpito na uokoaji, kuangalia suluhu za uhamishaji na kuweza kusuka mipango inayowapa wanajamii suluhu za muda mrefu ili kuwa na maisha mazuri.