Nchi mbalimbali duniani zinaendelea kupunguza utegemezi wao wa matumizi ya dola ya Marekani, hatua ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miongo kadhaa sasa.
Kupunguza matumizi ya sarafu hiyo kumehusishwa sana na nchi za kundi la BRICS (Brazil, Urusi, India, Uchina na Afrika Kusini), hasa kutokana na tishio la mara kwa mara la vikwazo vya dola na vita ya biashara.
Nchi nyingi zinazoendelea zimekuwa zikipambana na athari mbaya za kupanda na kushuka kwa thamani yake, na kuchochewa kupunguza utegemezi wa dola wakati zikijaribu kuweka sarafu zao sawa.
Dola yenye nguvu kwa ujumla inaumiza nchi zinazoendelea, ambazo hutegemea uwekezaji kutoka nje na mtaji wa nje, na kufanya iwe vigumu kwao kulipa madeni yao ya dola.