Ethiopia yapata mafunzo ya thamani kutokana na maendeleo ya China
2024-11-07 08:56:13| CRI

Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Umma na Kimataifa iliyo chini ya chama tawala cha nchini Ethiopia (PP), Bikila Hurisa amesema, mafanikio ya China katika kutafuta usasa kwa kuunda mfumo wa kipekee wa maendeleo yanaweza kutumika kama funzo kubwa kwa safari ya Ethiopia kuelekea ustawi.

Amesema China imefikia kiwango chake cha sasa cha maendeleo kwa kutafuta njia ya kisasa ambayo inaendana na umaalum wake na kwa kutumia mtaji wake wa nguvukazi.

Ujumbe wa ngazi ya juu wa viongozi waandamizi wa PP ulitembelea China hivi karibuni, ambapo wajumbe wa PP na wale wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) walifanya majadiliano kuhusu uhusiano kati ya vyama hivyo, kubadilishana uzoefu na kufanya semina ya mafunzo.

Bw. Hurisa amesema, mawasiliano ya hivi karibuni na wenzao wa China yamesaidia kuelewa vizuri juhudi za maendeleo ya China, ikiwemo mapendekezo mbalimbali ya maendeleo ya nchi hiyo, ikiwemo mipango ya miji na miradi ya maendeleo ya vijijini.