Mawaziri wa Afrika watathmini utekelezaji wa Azimio la Beijing la mwaka 1995 kuhusu usawa wa jinsia
2024-11-08 08:47:39| CRI

Mawaziri wa Afrika wamekutana ili kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa Azimio la Beijing na Jukwaa la Kuchukua Hatua, wakitoa wito wa juhudi za pamoja kukabiliana na vikwazo katika usawa wa kijinsia.

Mkutano huo uliowakutanisha mawaziri wa Afrika wenye dhamana ya kusimamia masuala ya jinsia na wanawake kama sehemu ya kamati ya kiufundi ya kitaalamu ya Umoja wa Afrika kuhusu usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake, umefanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia tarehe 6 hadi 7 mwezi huu.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Wanawake na Masuala ya Kijamii wa nchini Ethiopia Ergogie Tesfaye amerejea tena haja ya dharura ya kuhusisha suala la usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake katika maendeleo ya kitaifa na bara la Afrika kwa ujumla, na pia kwenye mikakati ya amani na usalama.

Naye naibu katibu mkuu na mchumi mwandamizi katika Tume ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa Bi. Hanan Morsy amesema, ni lazima kukabiliana na vikwazo vya usawa wa kijinsia na kuimarisha mifumo ya kitaasisi kwa ajili ya uwajibikaji ili kujenga hatma nzuri ya baadaye ambapo kila mwanamke anapata fursa ya kustawi.