Hivi karibuni Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilitoa tuzo ya elimu kwa watoto wa kike na wanawake kwa mashirika mawili ya Zambia na Uganda barani Afrika. Tuzo hiyo iliyoanzishwa na China kwa kushirikiana na UNESCO, ni tuzo pekee ya Shirika hilo inayosaidia kuboresha elimu kwa watoto wa kike na wanawake, na inachukua nafasi muhimu katika kutangaza nadharia ya usawa wa kijinsia katika elimu na masuala yanayohusisha vitendo vizuri, na pia katika kutekeleza usawa wa jinsia kama kipaumbele duniani. Tuzo hiyo inajumuisha fedha taslimu dola za kimarekani 50,000 kwa mwaka kwa mashirika mawili yanayofanya vizuri katika kuendeleza elimu kwa watoto wa kike na wanawake.
Linapokuja suala la elimu kwa mtoto wa kike, ni wazi kwamba halijapewa umuhimu wa kutosha, maana kipaumbele kwa wazazi ama walezi wengi ni kwa watoto wa kiume, huku watoto wa kike wakiachwa nyumba. Mpaka sasa, jumla ya watoto wa kike milioni 122 hawajaenda shule, na mbili ya tatu ya watu wazima ambao hawajui kusoma wala kuandika ni wanawake. Basi katika kipindi cha leo tutazungumzia kuhusu suala hili la elimu kwa mtoto wa kike na mwanamke.