Serikali ya Kenya imeanza mageuzi katika uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKlA) mjini Nairobi, ili kuongeza idadi ya abiria.
Waziri wa hazina ya taifa na mipango ya uchumi wa Kenya Bw. John Mbadi, amesema kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi, kuwa mageuzi hayo yatatoa huduma zisizo na changamoto, zenye ufanisi na staha kwa wateja wanaoondoka na kuwasili.
Amesema serikali imeweka kipaumbele katika teknolojia ya hali ya juu katika mageuzi ya kuboresha taratibu za forodha na uhamiaji ili kupunguza matumizi ya karatasi.
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ni moja ya vituo vitatu vikuu vya kuingilia nchini Kenya, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa, na wa Kisumu magharibi mwa Kenya. Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Kenya, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, Kenya ilipokea watalii laki 4.09 kupitia viwanja viwili vya ndege, huku laki 3.43 wakitumia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.