Maofisa wa Umoja wa Afrika (AU) na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi (Africa CDC), wamesema ushirikiano kati ya China na Afrika unaendelea kushika kasi kuelekea kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye ustahimilivu na mustakbali wa pamoja.
Maofisa hao wamesema hayo kwenye semina iliyofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, chini ya kaulimbiu ya "kujenga pamoja jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya".
Semina hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa mkutano wa FOCAC uliofanyika Septemba mjini Beijing, na kufafanua njia halisi za kujenga jumuiya hiyo yenye lengo la pamoja na kuheshimiana.
Mkurugenzi wa mahusiano ya nje na ushirikiano wa kimkakati wa Africa CDC Bibi Claudia Shilumani, amesema China na Afrika zinajenga mfumo wa afya wa kisasa unaoweza kuhimili na kukabiliana na changamoto za sasa za afya barani Afrika, na kuwaendeleza wafanyakazi wa afya wenye ujuzi ili kuhakikisha waafrika wananufaika na maendeleo ya usalama wa afya.