Mkutano mmoja wa kimataifa kuhusu kilimo cha mkataba barani Afrika ulianza jana Jumanne mjini Nairobi, ukiweka jukwaa kwa wataalamu wa kimataifa kujadili njia za kuimarisha ufanisi na ushirikishi wa kilimo cha mkataba barani kote.
Mkutano huo wa siku mbili umewaleta pamoja washiriki zaidi ya 200, wakiwemo maofisa wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi waandamizi wa serikali, wataalamu wa kilimo na wakulima kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Mchumi wa kitengo cha uchumi na sera za kilimo cha chakula katika Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Lan Li amesema kilimo cha mkataba kinaweza kutumika kama nyenzo ya kutekeleza viwango rafiki kwa mazingira, kwa kuwa makubaliano yanahusisha shughuli za kilimo zinazohimili mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa.