Tanzania kuimarisha uchunguzi na matibabu ya saratani kwa teknolojia ya nyuklia
2024-11-13 09:35:33| CRI

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amesema mipango inaendelea ya kuimarisha vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani kwa teknolojia ya nyuklia Tanzania bara na Zanzibar.

Rais Hassan amesema mpango wa kuimarisha vituo vya matibabu kwa nyuklia kudhibiti saratani, mbinu ambayo hutumia mionzi kusaidia kutambua na kutibu ugonjwa huo, utagharimu euro milioni 59.

Tangazo hilo limetolewa kwa niaba yake na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi wakati wa uzinduzi wa maabara na ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania katika visiwa vya Zanzibar. Rais Mwinyi amesema vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam, Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza na Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma vitaimarishwa.

Wizara ya afya ya Tanzania imesema watu elfu 44 hugunduliwa kila mwaka kuwa na saratani, na mwaka 2020 watu zaidi ya elfu 26 walikufa kwa ugonjwa huo.