Kenya imezindua kazi ya kuwawekea faru alama sikioni na kifaa cha utambuzi (transmitter) ili kuhimiza kazi ya uhifadhi wa wanyama hao.
Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya Bibi Rebecca Miano, amesema mpango huo utashuhudia vifaa vikiwekwa kwa faru 20 hadi 25 katika eneo la ulinzi la Tsavo Magharibi (lPZ) na hivyo kuimarisha ufuatiliaji na ulinzi wa wanyama hao walio hatarini.
Akiongea mjini Nairobi wakati wa kazi hiyo, Bibi Miano amesema kazi hii inaonyesha umakini wa Kenya katika kulinda moja ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani.
Mkurugenzi wa mamlaka ya wanyamapori ya Kenya (KWS) Bw. Erustus Kanga amesema kwa sasa idadi ya faru nchini Kenya ni 1,977, wakiwa ni pamoja na faru weusi 1,004 na faru weupe wa kusini 971, na wawili weupe waliobaki wa kaskazini.