Wataalamu wakutana Kenya kuhimiza matumizi ya ubunifu wa kidijitali ili kukuza sekta ya kilimo
2024-11-15 23:03:25| cri

Wataalamu wamekutana huko Nairobi, kuhimiza matumizi ya uvumbuzi wa kidijitali ili kukuza sekta ya kilimo barani Afrika.

Mkutano wa AgroWeb3 uliofanyika kwa siku moja umewaleta pamoja washiriki zaidi ya 200 wakiwemo maofisa wa shirika la Umoja wa Mataifa, wataalamu wa kilimo na wakulima kutoka kote barani Afrika, kuharakisha matumizi ya teknolojia kuimarisha uzalishaji.

Mkurugenzi wa kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika katika Shirika la Maendeleo ya Kilimo la Umoja wa Kimataifa (IFAD), shirika maalum la Umoja wa Mataifa, Bi. Sara Mbago-Bhunu amesema vyombo vya kidijitali ikiwemo majukwaa ya biashara ya kielektroniki vinaweza kuwasaidia wakulima kupata masoko mapya.

Amesema mifumo ya malipo ya kidijitali kama vile majukwaa ya sarafu za kielektroniki inaweza kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara ya bidhaa za kilimo, huku akiongeza kuwa majukwaa ya teknolojia ya kifedha pia yanaweza kukuwarahisishia wakulima kupata mkopo kununua pembejeo za kilimo.