Ofisi ya uratibu wa mambo ya binadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeripoti kuwa watu milioni 5.98 nchini Somalia watahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi mwakani, na idadi hiyo imepungua kwa asilimia 13 kuliko mwaka huu.
Ofisi hiyo imenukuu makadirio ya Mzunguko wa Mpango wa Kibinadamu wa 2025 (HPC) na kusema kati ya watu milioni 5.98 wanaohitaji msaada, washirika wa misaada watalenga watu milioni 4.6, idadi ambayo imepungua kwa asilimia 11 kutoka milioni 5.2 za mwaka huu.
Ofisi hiyo imesema kupungua huku kunaonesha mbinu kali zaidi ya kuweka wigo, kubainisha watu walioathirika na mishtuko inayochochea mahitaji ya kibinadamu.
Msukosuko wa kibinadamu nchini Somalia ni miongoni mwa changamoto ngumu zaidi duniani, wenye mchanganyiko wa migogoro ya ndani na majanga ya tabianchi ambayo husababisha watu kuhama na kukwamisha juhudi za maendeleo.