Rais Xi Jinping ahutubia mkutano wa 31 usio rasmi wa viongozi wa APEC
2024-11-17 11:38:37| CRI

Rais Xi Jinping wa China akihutubia mkutano wa 31 usio rasmi wa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) uliofanyika Jumamosi mjini Lima nchini Peru, alitoa wito kwa nchi za Asia-Pasifiki kubeba majukumu yao na kuhimiza kwa pamoja maendeleo ya eneo la Asia-Pasifiki wakati ushirikiano wa eneo hilo unapokabiliana na changamoto mbalimbali zilizoletwa na siasa za kijiografia, msimamo wa upande mmoja na sera za kujilinda kibiashara na kadhalika.

Rais Xi amependekeza kujenga muundo wenye uwazi na muunganiko wa ushirikiano kati ya nchi za Asia-Pasifiki. Amesema pande husika zinapaswa kuendelea kufuata mwelekeo wa uchumi wa wazi na mfumo wa pande nyingi,kushikilia kithabiti mfumo wa biashara wa pande nyingi wenye Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuwa kiini chake, kuamsha kikamilifu jukumu la APEC kama kiatamizi cha kanuni za uchumi na biashara duniani, na kukuza mafungamano ya kiuchumi na muunganiko wa kikanda,pia kubomoa kuta zinazozuia mtiririko huru wa biashara, uwekezaji, teknolojia na huduma,kuhakikisha utulivu na ufanisi wa mnyororo wa viwanda na ugavi, na kuhimiza mzunguko wa kiuchumi katika kanda ya Asia-Pasifiki na dunia kwa ujumla.

Aidha Rais Xi ametoa wito wa kuukuza ubunifu wa kijani kama msukumo wa ukuaji wa uchumi wa Asia-Pasifiki, akiongeza kuwa China inaendeleza nguvu mpya za uzalishaji kwa kuzingatia hali halisi na kuimarisha ushirikiano na pande husika katika ubunifu wa kijani. Amesema pande zote husika zinahitaji kutumia vizuri fursa zinazoletwa na duru mpya ya mapinduzi ya kisayansi na mageuzi ya kiviwanda, na kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika sekta za akili bandia, teknolojia ya Quantum Information, maisha na afya, na sekta nyingine nyingi za mstari wa mbele. China itazindua Pendekezo la Ushirikiano wa Mabadilishano ya Data Duniani, na kutafuta ushirikiano wa kina na pande mbalimbali ili kukuza mabadilishano hayo yawe salama,rahisi na yenye ufanisi.

Rais Xi pia amependekeza kujenga dhana ya maendeleo ya Asia-Pasifiki yaliyo shirikishi na yanayonufaisha wote. Ametoa wito kwa pande husika kutumia vyema jukwaa la APEC,kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi,na kuongeza uungaji mkono kwa nchi zinazoendelea na nchi zilizo nyuma kiuchumi, ili matunda ya maendeleo yazinufaishe nchi nyingi zaidi na watu wengi zaidi.

Rais Xi amesema kuwa maendeleo ya China yatatoa fursa nyingi mpya kwa eneo la Asia-Pasifiki na dunia nzima, akiongeza kuwa China inakaribisha pande zote kuendelea kupanda “treni ya mwendokasi”ya maendeleo ya China, kusonga mbele pamoja na China na kufanya juhudi pamoja na China kwenye safari ya kujenga dunia yenye amani, maendeleo, ushirikiano na ustawi wa pamoja.  

Kwenye mkutano huo,Rais Xi pia ametangaza kuwa China itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa APEC wa 2026.