Changamoto za Watoto kuacha shule
2024-11-23 09:00:03| CRI

    Inafahamika kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, na wazazi na walezi wengi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wao wanapata elimu tena iliyo bora ili kuwajengea msingi imara kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Wazazi wamekuwa wakijitoa kwa hali na mali kuhakikisha watoto wao wanasoma katika shule zilizo bora ili tu kuhakikisha watoto wao wanafaidika na elimu na kuwa katika njia sahihi ya kuwa na maisha bora katika siku zao z baadaye. Lakini baadhi ya wakati, watoto haohao wanaamua kuacha shule kwa sababu na visingizio mbalimbali. Watoto wa kike wanajikuta wameachishwa masomo na wazazi wao kwa lengo la kuwaoza na kujipatia mahari hivyo kuinua ngazi ya maisha ya familia, wengine wanajikuta wakiacha kusomeshwa na wazazi wao na badala yake wenzao wa kiume kuendelezwa kielimu kwa madai kuwa, mtoto wa kike ataolewa na kwenda kwa mume wake hivyo hakuna haja ya kumsomesha, na wengine kwa bahati mbaya wanapata ujauzito wakiwa bado shuleni na hivyo kukatiza masomo yao.

    Kwa upande wa watoto wa kiume, wengi wao huanza kufanya kazi za vibarua ambazo zinawaingizia kipato kidogo, na hivyo kuona hakuna haja ya kuendelea na shule. Lakini kuna wengine ambao wanajiona hawana uwezo kama wenzao, na hivyo wanakata tamaa ya kuendelea na masomo na kuamua kujiajiri. Leo katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake, tutaangalia zaidi suala hilo la sababu ambazo zinawafanya watoto kuacha shule.