White House yakiri Marekani haina vifaa vya kutosha vya kupima Virusi vya Corona
Ikulu ya Marekani imethibitisha kuwa nchi hiyo haina vifaa vya kutosha vya kupima virusi vya corona huku viwango vya maambukizi vikiendelea kuongezeka.
Makamu wa rais Mike Pence amesema utawala wa Trump hautaweza kufikia malengo yake ya kutoa vifaa milioni moja vya kupima virusi hivyo wiki hii.
Huku hayo yakijiri bunge la Marekani limeidhinisha kwa haraka isiyokuwa ya kawaida kupatikana kwa vifaa hivyo kwa dharura ili kukabiliana na mlipuko wa corona.
Kimataifa, mamlaka zimethibitisha zaidi ya visa 92,000 vya virusi hivyo.
Visa zaidi ya 80,000 vimeripotiwa- China, ambako ni chimbuko la virusi hivyo. Duniani , zaidi ya watu 3,000 wamefariki kutokana na ugonjwa huo.
Idadi ya vifo vilivyotokana na virusi vya corona nchini Marekani imeongezeka hadi 12 siku ya Alhamisi, visa vingi vikiripotiwa katika jimbo la kaskazini magharibi la Washington.
Kufikia sasa zaidi ya visa 200 vya Covid-19 vimeripotiwa katika majimbo 20 ya Marekani.
Katika jimbo la Washington, maafisa katika eneo la Seattle wametangaza visa 20 vipya vya virusi vya corona, na kufikisha 70 idadi ya visa vilivyoripotiwa, kwa mujibu wa idara ya afya katika jimbo hilo.
Watu tisa waliofariki Marekani kufikia sasa wote walikuwa wamezuiliwa katika kituo kimoja cha afya viungani mwa Seattle, ambayo sasa inachunguzwa na mamlaka ikiwa ilifuata muongozo wa kudhibiti na na kuzuia maaambukizi.
Baadhi ya makampuni makubwa katika eneo hilo ikiwa, ni pamoja na Microsoft na Amazon, yamefunga huduma zao au kuwashauri wafanyikazi wao kufanya kazi wakiwa nyumbani.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |