Morocco yamtuhumu mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika kwa kuzuia ombi lake la kujiunga tena na Umoja huo
Morocco imemtuhumu mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Bi. Nkosazana Dlamini-Zuma kwa kuzuia ombi lake la kujiunga tena na Umoja huo.
Gazeti la kila siku nchini humo Le Matin limenukuu taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo inayosema, Morocco haijafurahishwa na vitendo vinavyofanywa na mwenyekiti huyo vya kuzuia uamuzi wa Morocco wa kuchukua tena nafasi yake halali ndani ya Umoja wa Afrika.
Taarifa hiyo imesema, nchi nyingi wanachama wa Umoja huo zinaunga mkono Morocco kurejea kwenye Umoja huo, na kwamba tayari nchi hizo zimewasiliana na Bi Dlamini-Zuma na kuwasilisha barua rasmi na halali zinazounga mkono Morocco kurejea kwenye Umoja huo katika mkutano ujao.
Mwezi Septemba, Morocco iliwasilisha rasmi ombi la kujiunga tena na Umoja wa Afrika ambao nchi hiyo ilijitoa miaka 32 iliyopita.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |