Rais wa Nigeria arejea nyumbani
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari Ijumaa ya wiki hii amerejea nchini mwake, baada ya kuwa nje ya nchi kwa majuma kadhaa, ambapo alikuwa akipatiwa matibabu nchini Uingereza, hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo.
Buhari mwenye umri wa miaka 74, na ambaye alichukua usukani kuongoza nchi hiyo mwaka 2015 mwezi Mei, aliondoka mjini Abuja Januari 19 mwaka huu, kwaajili ya matibabu nchini Uingereza.
Awali alikuwa amepanga kukaa nchini Uingereza kwa muda wa siku 10 lakini akalazimika kuongeza muda wa kukaa huko baada ya kushauriana na madaktari wake wanaomtibu, hali iliyozusha sintofahamu zaidi kuhusu afya yake.
Taarifa ya ikulu iliyotolewa Alhamisi ya wiki hii imesema Rais Buhari ametoa shukrani kwa raia wote wa Nigeria wanaoishi nchini humo na nje ya nchi kwa kumuombea, ikiongeza kuwa kuongeza kwake muda kusalia nchini Uingereza kulitokana na ushauri wa madaktari.
Hata hivyo taarifa hii ya ikulu haikuweka wazi taarifa za kina kuhusu kilichokuwa kikimsumbua rais Buhari.
Mapema siku ya Alhamisi, idara ya habari ya ikulu ya Nigeria, ilichapisha kwenye mtandao, picha ikimuonesha rais Buhari akisalimiana na askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Justin Welby jijini London.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |