Rais Xi Jinping atangaza hatua mpya za China katika kufungua mlango kwenye ufunguzi wa CIIE
Rais Xi Jinping wa China amehudhuria na kutoa hotuba kwenye Maonesho ya kwanza ya kimataifa ya uagizaji bidhaa ya China yaliyofunguliwa leo mjini Shanghai. Rais Xi ametangaza kuwa China itaongeza hatua za kufungua mlango, akisisitiza kuwa mafungamano ya kiuchumi duniani ni mwelekeo usiozuilika, nchi zote zinatakiwa kuhimiza ufunguaji mlango na ushirikiano, ili kupata maendeleo kwa pamoja. Pia amesisitiza kuwa China haitasimamisha hatua zake katika kuhimiza ufunguaji mlango katika kiwango cha juu zaidi, kujenga uchumi ulio wazi kwa dunia, na kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.
Maonesho ya kimataifa ya uagizaji bidhaa ya China ni maonesho ya kwanza ya kitaifa yanayohusu uagizaji wa bidhaa duniani, ambayo yanafanyika kwa kufuata pendekezo la rais Xi Jinping wa China. Maonesho hayo ya kwanza yameshirikisha nchi, sehemu na mashirika ya kimataifa 172, viwanda zaidi ya 3,600 duniani, pamoja na wafanyabiashara zaidi ya laki 4 kutoka China na nchi za nje.
Rais Xi Jinping akihutubia ufunguzi wa maonesho hayo, ameeleza kuwa kufanyika kwa maonesho hayo ni uamuzi muhimu wa China katika kuhimiza ufunguaji mlango kwa kiwango cha juu zaidi, pia ni hatua muhimu ya China ya kufungua soko kwa dunia nzima.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |