Wabunge wa Uingereza wapinga mkataba wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya
Wabunge wa Uingereza wamefutilia mbali mkataba wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya uliofikiwa kati ya serikali ya Theresa May na Umoja wa Ulaya. Dakika chache kabla ya kura hiyo kupigwa, Waziri Mkuu Theresa May amewaomba wabunge kuheshimu matokeo ya kura ya maoni.
Kukataliwa kwa mpango huo ni pigo kubwa kwa Theresa May na serikali yake. Wabunge hawakujali ahadi iliyotolewa na Theresa May ya kufanya kazi kwa karibu zaidi na bunge wala wito kwa viongozi waliochaguliwa kutosaliti uamuzi wa wawanchi wa Uingereza kupiga kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Wabunge wamekataa mpango wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya kwa kura 432 dhidi ya 202.
Ingawa sio mshangao, kushindwa kwa Theresa May kunaongeza wasiwasi unaoendelea kuikumba Uingereza kwa sasa. Pia inatoa tumaini kwa wengine.
Uamuzi wa wabunge umekaribishwa na wafuasi wanaotaka kupigwa kura mpya ya maoni.
Hivi karibuni wanasiasa mbalimbali walitoa wito wa kufanyika kwa kura mpya ya maoni ili kuondokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea.
Hata hivyo serikali ya Theresa May ilifutilia mbali hoja hiyo, ikisema itazidisha mgawanyiko na kukiuka uamuzi wa wananchi wa Uingereza ambao walipiga kura Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya mnamo mwaka 2016.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |