Kabila la Buyi lililopo Kusini mwa Guiyang lipo mstari wa mbele kuendeleza mila na utamaduni wa kabila hilo
1. Katika majadiliano ya kipindi kilichopita ulisema uliwahi kutembelea baadhi ya sehemu wanazoishi makabila madogomadogo sasa unaweza kutuelezea sehemu hizo?
Ahsante sana kwa kweli baadhi ya makabila haya madogomadogo yanapatikana Kusini mwa mji wa Guiyan ambapo kuna kijiji cha Matou, Shuitou na Ping. Kwenye vijiji hivi wanaishi watu wa kabila dogo la Buyi. Na kabila hili bado linafuata utaratibu uliokuwa ukifuatwa na babu zetu kwa karne nyingi zilizopita.
2. Kawaida makabila mengi madogomadogo huwa yana mtindo wao maalum wa kumkaribisha mgeni na je mlipata makaribisho ya aina gani mlipofika huko?
Kama kawaida mgeni anapoingia mahali popote hukaribishwa, na kwa upande wa kabila hili mgeni hukaribishwa kwa wimbo maalumu na baadae mgeni huyo hupewa mvinyo wa kienyeji uitwao Biangdang ambao unatengenezwa na watu wa kabila hilo, mvinyo huo unatengenezwa kwa kutumia mchele.
Baada ya hapo mgeni hukaribishwa tena kwa dansi maalum, ambapo wanaume wanapiga miti ya mianzi na wanawake wanacheza kwa kuruka na kufuata hatua maalum.
Vyakula vingi katika vijiji hivyo vinatengenezwa na wao wenyewe mfano wanatengeneza tofu kwa kutumia unga wa mchele, mchele ambao unatokana na mpunga wanaolima wenyew
Wakati wa chakula unapowadia wenyeji wa kabila hili huwaimbia wimbo wageni huku wakiwa na mvinyo mkononi hapo huwa wanaombewa Baraka, mvinyo huo hunywewa kwa vikombe viwili viwili kwa mujibu wa mila zao ukinywa viwili vinawakilisha miguu miwili, ukinywa vinne ina maana utapata pesa kwa miongo au majira manne, ukinywa sita maana yake mambo yako yote yatakuwa sawa na hutokuwa na matatizo, na ukinywa vikombe nane utakuwa tajiri, vikombe kumi vinakuhakikishia kupata bahati na ukinywa 12 maisha yako yatakuwa na mwisho mzuri.
3. Je wenyeji wa vijiji hivi wanajishughulisha na kazi gani?
Wenyeji wa vijiji hivi wanajishughulisha na kazi za ukulima na ufugaji. Mpunga na mahindi ni mazao makubwa sana yanayolimwa hapo, mbali na mazao hayo pia wanalima matunda na mboga. Kwa upande wa ufugaji wanapendelea sana kufuga kuku, bata na ng'ombe.
Mazao ya mpunga hukobolewa kwa mashine maalum inayotumia nguvu ya maji.
Sherehe kubwa ambazo zinasherehekewa kila mwaka ni mbili kila ifikapo tarehe 30 mwezi wa tatu na tarehe 6 mwezi wa sita kila mwaka.
4. Mbali ya ufugaji na kilimo je wanavijiji wa huko wanafanya shughuli gani zaidi.
Baadhi ya wanakijiji huwa wanajishughulusha na uwekezaji mfano kwenye kijiji cha Shuitou kuna hoteli ambayo ina hadhi ya kimataifa, hoteli hii inapokea wageni kutoka nchi mbalimbali kama vile nchi za bara la Ulaya,Asia na Afrika. Huduma zote muhimu zianapatikana kwenye vyumba vya hoteli hiyo.
5. Kwa upande wa sherehe za harusi huwa wanaandaa kama kawaida au kuna tofauti kidogo
Matauarisho ya harusi zao hazina tofauti kubwa ukilinganisha na harusi za kawaida kwani karibu na kipindi cha harusi bwana harusi ndie anayetayarisha kila kitu cha kwenye nyumba, kama vile kununua kitanda, viti makochi n.k. Na kawaida siku ya harusi huwa wanalishwa njugu mbichi bibi na bwana harusi ili vizazi vyao viwe na nguvu na uwezo mkubwa. Na baadae husujudu mbele ya wazazi wao ili wapate Baraka na hapo husindikizwa hadi nyumbani kwao.
Ingawa watu wengi huwa hawapendi kuendeleza utamaduni kwa kuona kuwa hayo ni mambo ya zamani lakini kabila hili liko mstari wa mbele kuendeleza utamaduni wa kabila hili.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |