Kenya imetangaza kuwa inawaondoa wanajeshi wake kutoka kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani Sudan Kusini, siku moja tu baada ya kamanda wake kufutwa kazi na Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-moon
Ban Ki-moon alimfuta kazi Luteni Kanali Johnson Ondieki baada ya ripoti ya uchunguzi kusema alikosa kuwajibika kulinda raia mapigano yalipozuka upya nchini Sudan Kusini mwezi Julai.
Inadaiwa kwamba walinda amani waliokuwa chini ya jemedari huyo hawakuchukua hatua yoyote wanajeshi wa serikali waliposhambulia kituo cha utoaji misaada mjini Juba na kuwadhulumu raia.
Wakati huo huo Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametetea hatua ya nchi yake na kuwaondoa wanajeshi wake kutoka kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Sudan Kusini.
Rais Kenyatta alisema kuwa Kenya imejitolea katika kuchangia amani katika kanda hii na dunia nzima lakini akaongeza kuwa heshima ya nchi haiwezi kuchafuliwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |