Watu 38 wakamatwa Niger baada ya vifo vya wanakijiji 18
Nchini Niger, watu 38, wengi wao wakiwa vijana wakulima , walikamatwa na polisi baada ya vifo vya wanakijiji 18 Jumanne wiki hii.
Mapigano yalizuka kati ya wakulima na wafugaji karibu na wilaya ya Bangui, mkoani Tahoua magharibi mwa nchi yakisababisha watu zaidi ya 40 kujeruhiwa.
Yote yalianza Jumanne asubuhi wakati ng'ombe waliposhambulia shamba la nafaka. Katika mabishano yaliyofuata mmiliki wa shamba aliuawa. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Ndani imesema kuwa kulitokea 'purukushani'.
'Purukushani' kati ya wakulima na wafugaji kutoka jamii ya Peul ambazo zilisababisha vifo vya watu 18, ikiwa ni pamoja na 7 waliochomwa moto wakiwa hai, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, wengine 43 wakijeruhiwa na nyumba 22 kuchomwa moto.
Wanawake na watoto mia moja na ishirini na tatu waliotishiwa na wauaji waliwekwa haraka chini ya ulinzi wa polisi.
Migogoro hii inatokea mara kwa mara nchini Niger, hasa wakati wa kipindi cha mavuno ambayo pia kinaendana sanjari na kipindi cha kupeleka mifugo katika maeneo makubwa ya malisho.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |